Saturday, September 10, 2011

MELI IMEZAMA UNGUJA NA ABIRIA ZAIDI YA 610 WAHOFIWA KUFA ALAFAJIRI YA LEO

Pichani Meli ya LCT Islanders ikiwa imezama Pwani ya Nungwi, Unguja. Picha kwa hisani ya Zanzinet.

Meli ya LCT SPICE ISALNDERS imebinuka na kuzama katika Bahari ya Hindi huko Pwani ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati ikielekea Pemba.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu wa Zanzibar, Mhe. Haji Issa Ussi akithibitisha tukio hilo amesema kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa nane na nusu usiku wa kuamkia leo ikiwa imebeba abiria 610 pamoja na mizigo. 

Mhe. Ussi amesema kuwa meli hiyo iliondoka Bandari ya Malindi Unguja ikiwa katika hali ya uzima kabisa lakini katikati ya safari ikatokea hitilafu na kusababisha kubinuka na hatimaye kuzama. Hadi sasa bado haijafamika idadi kamili ya watu waliofariki katika ajali hiyo lakini vyombo vya uokozi vimefika katika eneo la tukio ili kutoa msaada.

 Naibu Waziri huyo amesema Serikali kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya usafiri binafsi vya boti ziendazo kasi zimekwenda katika eneo la tukio kutoa msaada unaohitajika, hali kadhalika Jeshi la Polisi limetuma Helikopta yake kwenye eneo la tukio.

 Awali, Mhe Ussi amesema kuwa mamlaka zinazohusika zilipata taarifa za kuzama kwa meli hiyo baada ya Meli nyingine ya MV Jitihada inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuripoti kuzama kwa meli ya Spice Islanders ambayo nayo ililazimika kukatisha safari yake ili kuelekea Kisiwa cha Pemba na kwenda kwenye tukio.

Serikali imewaomba wanananchi kuwa watulivu na taarifa zaidi zitakuwa zikitolewa kuhusiana na ajali hiyo kwa ujumla.

Habari hizi ni kwa Hisani ya Blogu ya Issa Michuzi

No comments:

Post a Comment

Unaonaje hii?